Kumbukumbu la Torati 2:
π€ Fungu la kwanza la sura hii linabeba miaka yote ya Waisraeli kuzunguka jangwani. Bwana akawaelekeza sasa kuelekea Kaskazini kwa kuona kuzunguka kwao kumetosha.
π€ Katika kwenda kwao walitarajiwa kupita Seiri walipokaa watoto wa Esau pamoja na nchi ya Wamoabi walipokaa watoto wa Lutu. Bwana aliwazuia Israeli kufanya chochote kwa mataifa haya mawili kwa kuwa Bwana aliwapa ardhi hizo baba wao.
π€ Kuelekea Kaskazini zaidi Waisraeli walitakiwa kupita nchi ya Waamori. Haukuwa mpango wa Mungu kuwadhuru watu hawa endapo kama wangewaruhusu Israeli kupita katika nchi yao. Lakini Musa alipotuma ujumbe kuomba kupita, mfalme Sihoni alikataa na kujiandaa kwa vita na kuja kuwakabili Israeli.
π€ Bwana akamthibitishia Musa kwa kusema _”Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano.”_
π€ Ingawa taifa hili lilikuwa la waabudu sanamu lakini kikombe chao kilikuwa hakijajaa bado. Lakini kwa kuwachokoza Israeli kikombe chao kikajaa hakika naye Bwana akawaadhibu. Watu hawa walikuwa wameshuhudia mambo makubwa ya Bwana Mungu wa Israeli kuweza kuwanyenyekeza. Waliona jinsi Israeli walivyoongozwa na Mungu kupita katika mataifa mengine kwa amani na kwa hofu kuu. Walifahamu namna Bwana alivyowatoa Misri kwa mkono hodari na kuwaongoza jangwani. Waliona jinsi mfalme wa Ardi alivyoadhibiwa na Bwana kwa kuwashambulia Israeli (Hesabu 21). Pamoja na yote haya walimkaidi Bwana.
π€ Kwa upande mwingine pengine huenda historia iliwapumbaza na kuona ya kuwa Mungu wa Waisraeli wanammudu. Miaka 40 iliyopita waliwapiga Israeli vilivyo pale walipojaribu kupanda wenyewe bila Bwana baada ya kumuasi Bwana na kuadhibiwa kurudi jangwani.
π€ Watu hawa walikuwa na miili mikubwa (majitu), majeshi hodari na miji yenye ngome kubwa. Miaka 40 iliyopita wana wa Israeli walipotumwa kuipeleleza nchi waliona watu hawa na kuogopa sana, na kujiona mapanzi mbele yao. Kwa mara nyingine wana wa Israeli walikuja kukabiliana tena na kile kilichowashida baba wao.
π€ Waisraeli walipata hofu lakini walimwona Musa akiwa thabiti naye akawaambia _”BWANA asema, Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako; anza kuimiliki, upate kuirithi nchi yake.”_ Kumb la Torati 2:31. Na walipotazama wingu la Bwana lipo pamoja nao, wakapata ujasiri ya kuwa hii ndiyo njia Bwana aliyoichagua waienende.
π€ Kwa ujasiri mkubwa wakampiga mfalme Sihoni na kutwaa miji yake yote. Wakawaua watu wake wote pamoja na kutwaa mali. Jambo lililowashinda baba wao, watoto wao wakaliweza.
*Masomo:*
π Wokovu wetu hautegemei kiwango cha miujiza tuliyoshuhudia bali namna tunavyojisalimisha mioyo yetu. Kizazi kilichofia jangwani kilikuwa kimeshuhudia miujiza mingi na mikubwa ya Bwana tangu kutoka Misri hadi kufika mpaka wa Kaanani. Lakini bado walimtilia Mungu mashaka, ukilinganisha na kizazi hiki kilichozaliwa jangwani ambacho hakikuwa kimeona mengi kulinganisha na baba wao, lakini waliamini. _”Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”_ Waebrania 11:1.
π Ushawishi wa kiongozi ni nguzo imara ya mafanikio. Uthabiti wa Musa na imani yake viliwaondoa mashaka Waisraeli juu ya vita iliyokuwa inawakabili punde. Je, mvuto wako kwa wengine una ushawishi wa aina gani?
π Umejengaje uhusiano wako na Mungu, kiasi cha kuweza kuitambua sauti yake katika maisha yako?
Bwana akubariki unapojifunza zaidi.
ππΎ ππΎ ππΎ ππΎ
Post A Comment:
0 comments: