Leo Tunaanza Kitabu cha Kumbukumbu la Totari
Utangulizi:
✍๐พ Kitabu cha Kumbukumbu la Torati ni kitabu cha mwisho katika vitabu vitano vya Musa. Maudhui makubwa ya kitabu hiki ni kuwakumbusha Waisraeli juu ya sheria za Mungu.
Kitabu hiki kimegawanyika katika maeneo makuu yafuatayo:
▪Hotuba ya kwanza ya Musa (Kutoka 1-4).
▪Hotuba ya Pili ya Musa (Kutoka 5-28).
▪Hotuba ya Tatu ya Musa (Kutoka 29-30).
▪Matukio ya Mwisho ya Utumishi wa Musa na Kifo chake (Kutoka 31-34).
〰〰〰〰〰〰〰〰〰〰〰〰
*Kumbukumbu la Torati 1:*
✍๐พ Mwezi mmoja kabla ya kufariki kwake, Musa anawakumbusha wana wa Israeli safari yao ilivyokuwa kwa kipindi cha miaka 40. Kwa dhati ya moyo wake nabii mzee akifahamu yeye hatoingia nao nchi ya ahadi, anawiwa na mzigo wa kuwausia taifa hili la kizazi kipya. Kuwaelezea safari yao ilivyokuwa, changamoto zake na mafanikio yake.
✍๐พ Anaanza kwa kueleza uhalisia kuwa safari yao kutokea Mlima Horebu mpaka Kadesh-barnea ilipaswa kuwa fupi mwendo wa siku zisizozidi 11 katika hali ya kawaida, ingawa wao iliwachukua muda wa miaka 40. Anakielezea kizazi hiki kipya sababu ya safari hiyo kuwa ya muda mrefu kiasi hicho ili iwe fundisho kwao.
✍๐พ Anaeleza agizo la Bwana kwa Waisraeli kuanza safari kuelekea nchi waliyoahidiwa baba zao Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Katika maelezo yake Musa anaelezea namna ambavyo ilibidi Kuweka mfumo mzuri wa uongozi wa uwakilishi katika safari hiyo. Uongozi ulipangwa kuanzia makumi na kuendelea kutokana na _Bwana kuwa amewafanya kuwa wengi, mfano wa nyota za mbinguni._ Jambo la kuvutia katika hotuba yake ni namna ambavyo Musa anaonesha alivyokuwa na mtizamo chanya huku akihusisha vyema matukio ya wana wa Israeli na uongozi wa Mungu.
✍๐พ Musa anasimulia namna Bwana alivyowaongoza _”katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha”_ kuelekea nchi ya vilima vya Waamori, nao wakafika Kadesh-barnea. Naye akawaagiza, _”Mmefika nchi ya vilima vya Waamori, anayotupa sisi Bwana, Mungu wetu. Tazama, Bwana, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike.”_
✍๐พ Katika hatua hiyo watu *hawa* wakamshauri kuwa, kabla hawajaingia kwanza wakaipeleleze nchi, naye akavutiwa na wazo hilo. Hata hivyo, ushauri huu ulibainika kuwa mbaya hapo baadaye. Ingawa Musa anaongea na kizazi kipya kabisa ambacho hakikuwepo wakati huo, lakini anazungumza nao kana kwamba ni wao ndio waliotenda, hii ni dhana ya kuwajibika pamoja _(collective responsibility)._
✍๐พ Katika kusimulia taarifa iliyoletwa na wapelelezi wale, Musa hakuwalaumu wapelelezi walioleta habari mbaya, bali mkutano kwa kukosa imani kwa Bwana na hivyo kufanya uchaguzi mbaya. Tazama katika kueleza kwake Musa anasema _” wakatuletea habari wakasema, nchi hii anayotupa Bwana, Mungu wetu, ni nchi njema. Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la Bwana, Mungu wenu; mkanung'unika hemani mwenu.”_
✍๐พ Ni kawaida kwa hulka ya kibinadamu kukwepa kuwajibika kwa makosa tunayofanya wenyewe. Kauli za kama: nilishauriwa vibaya, sikujua, hukuniambia, n.k tumezitumia mara nyingi kutufanya tuhisi vizuri kwenye jambo ambalo kwa uhalisia tuna hatia nalo. Watu hawa bila shaka walidai walimuasi Bwana kutokana na taarifa mbaya iliyoletwa na wapelelezi waliokuwa wengi (10 kati ya 12). Hata hivyo, kwa Musa hakukuwa na udhuru katika uamuzi mbaya uliofanywa na watu kwa kuwa agizo la Bwana lilikuwa liko wazi kwao.
✍๐พ Pamoja na Musa kuwaonya _”wasifanye hofu, wala wasimwache Bwana, Mungu wao, aliyetangulia mbele yao, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yao; na huko jangwani, walipoona alivyowachukua Bwana, Mungu wao, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote waliyoiendea, hata wakafikilia mahali pale. Lakini katika jambo lile hawakumwamini Bwana, Mungu wao, aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonesha njia watakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zao.”_ Pamoja na yote hawakutii, bali walimuasi Bwana.
✍๐พ Kama matokeo ya uasi wao, walichelewa kuingia nchi ya ahadi kwa miaka hiyo 40. Sababu ya kuwaambia kizazi hiki kipya habazi hizi ni kwa sababu wao pia walikuwa na fursa ya kumcha Bwana na kuwa warithi sawa sawa na ahadi yake au kumuasi Bwana na kaudhibiwa kama baba zao.
*Masomo:*
๐Yeye asiyejifunza kutokana na historia ana hatari ya kuirudia.
๐Kufanikiwa au kutofanikiwa kwa kundi kunategemea sana uwajibikaji wa pamoja _(collective responsibility),_ kufanya sehemu yetu kwa uaminifu kunaweza kuepusha matokeo yasiyotakiwa, tofauti na hapo tuwe tayari kuhusika pia kwa matokeo ya kutowajibika kwetu.
๐ _“Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.”_ Yohana 9:41. Kukwepa kuwajibika katika jambo hakubadilishi ukweli huo, sana sana kunaondoa fursa ya mhusika kujitafakari na kupata fursa ya kujisahihisha.
Mungu akubariki sana.
๐๐พ๐๐พ๐๐พ๐๐พ
Post A Comment:
0 comments: