© www.mwakasege.org 

3️⃣SEMINA YA KUPANDA NA KUVUNA-TUGHIMBE HALL MBEYA. 26 JANUARI 2020.

NA MWL CHRISTOPHER MWAKASEGE 


Tunaendelea tulipoishia na Jambo la pili,  Leo tuendelee na la tatu.

JAMBO LA TATU. 

USITOE SADAKA KWA AJILI YA AKIBA YAKO PEKE YAKO.

Mithali 15:6a
“Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;”

Mwenye haki ni yule ambaye yuko ndani ya Kristo.Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake, amehesabiwa haki bure ya kusimama ndani yake na mbele za Mungu kama vile hajawahi kufanya kosa. 

Kwa hiyo unapokuwa ndani ya Yesu Kristo unatakiwa kuwa na akiba nyingi. uwe na akiba ya pesa, ya mazao, ya matendo, n.k. Unakuwa na akiba nyingi ili usizitumie peke yako. 

Mithali 13:22a
“Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;”

Wengine wanakula akiba zao mpaka hela za kuwazikia zinaisha kabisa. Watoto wanaenda kukopa kutengeneza mazishi. Biblia inataka wazazi wawaachie wajukuu. 

Huu mstari ulinitesa sana wakati nausoma kwa ajili ya kutengeneza akiba ya wajukuu. Nimesoma kidogo masuala ya uchumi darasani na nilipookoka nikaona hali yetu ya uchumi ilipata shida, ilinisumbua sana. Ndipo Mungu akaniambia mfumo wa uchumi wake na tulionao humu Duniani ni tofauti. 

Mungu akaniambia “kwa mfumo wa kwenu Duniani msipofuata maagizo Yangu hamwezi mkafanikiwa; mkiufuata mfumo wa kwangu mtafanikiwa huko Duniani.”

Ndipo nikaanza kusoma Biblia na nikaona vitu vingi kuhusu akiba na mojawapo ni cha wajukuu kuwa natakiwa kuweka akiba kwa ajili ya wajukuu. 

Biblia inasema wazazi wanatakiwa waweke akiba kwa ajili ya watoto na sio watoto kuweka akiba kwa ajili ya wazazi. Lakini wazazi sasa tunategemea akiba waliyoweka watoto. 

Hapa simaanishi watoto wasiwasaidie wazazi. Hapa najaribu kuongea na wazazi wenye watoto na wazazi watarajiwa kuwa ili waanze kujipanga mapema. 

Biblia iko wazi kabisa kuwa 
Mithali 19:14
“Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA.”

Maana yake ukiozesha kijana, unatakiwa umpe na nyumba na kama binti anaolewa kati ya zawadi mojawapo Biblia inategemea kuwa iwe ni nyumba kama sio nyumba, iwe ni kiwanja. Haya yote Biblia imesema. 

Hili somo lilitutesa sana mimi na mke wangu kwa sababu wakati huo tulikuwa na pesa ndogo sana kwenye miaka ile ya 1980s sasa je hiyo akiba unaweka wapi? Kwa hela ipi? 

Lakini mstari unabaki pale pale uwe maskini, uwe tajiri, umefilisika au haujafilisika ukisoma huo mstari muda wowote utakuta uko vivyo hivyo. Ukikasirika sana, huo mstari unabaki kuwa kama kioo hata ufanyeje. 

Watu wengine wakishaona uchumi umekuwa mgumu sana wanaacha kusoma Biblia kwa sababu kila wakisoma wanakutana yale maneno yakiwapiga ngumi. Kuna muda wananyoosha mikono na kuacha kabisa kuisoma na wakikuta kwenye Biblia sehemu inayoongelea baraka atasema hiyo mistari ni kwa ajili ya wengine nakujisemesha kuwa maisha hayo yanamtosha na ameridhika nayo. 

Na kujisemesha kuwa duniani hatuna mji udumuo bali ni wapitaji tu  (Waebrania 13:14), pia kuwa mbinguni hatuendi na kitu. 

Unaweza ukasimama na mistari yote inayokutetea kuhusu uchumi lakini bado njaa ikikubana utaenda sokoni kununua na wakati huo hela huna. 

Inapofika kwenye masuala ya kuweka akiba ni lazima ufikiri vizuri, huwezi kuweka akiba kwa ajili yako peke yako, Yusufu alipopewa hekima na Mungu aliweka akiba zaidi ya kile walichokihitaji, alitakiwa akusanye sehemu ya tano ya mavuno yote, kwa hiyo alipiga hesabu ya mavuno yote, kilo ngapi,au tani ngapi, kwa hiyo wanatafuta sehemu ya tano ambayo ni sawa 20%, 

Wanaweza kutunza 20% na mara saba maana yake 140% kwa hiyo ni 100% + 40% juu yake, njaa haikuikumba tu Misri bali Kanaani na  dunia yote na nchi zote zilizofahamika wakati ule na ilipotokea njaa Yusufu akafungua maghala na watu wa nchi mbali mbali walienda kununua, alikuwa na akiba ya kuwatunza watu wote wa Misri kwa miaka 7 na watu wote kutoka nchi zingine hawakunyimwa.

Kulikuwa na 40% na unapowatazama wale Wananchi wa Misri walikuwa na hali ngumu sana kwa sababu mwaka wa pili walikuwa wameishiwa kila kitu mpaka hela lakini Mungu hakusema wekeni


kiba ya hela kwa sababu hazitaweza kununua sokoni alisema weka akiba ya nafaka.

Mungu hawezi kukupa Roho Mtakatifu kukusaidia kuweka akiba kwa ajili yako mwenyewe peke yako kwa sababu anajua kuna wengine wataponea mikononi mwako kuna watu kwenye familia yako wataponea mikononi mwako, majirani wataponea mikononi mwako, kuna watu wageni kabisa wataponea mikononi mwako kwa sababu Mungu amekuheshimu una nidhamu anaweza kukupa kitu hutakula, hutamnyima ambaye Mungu atahitaji umpe.

Isaya 58:12
Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.

Kumbuka 
1 Timotheo 6:19 inasema 
Huku wakijiwekea msingi mzuri wa akiba kwa ajili ya maisha ya baadae

Kwa hiyo akiba ni msingi mzuri kwa ajili ya maisha ya baadae. Mungu anapokupa akiba kumbuka si tu kwa ajili ya maisha ya baadae peke yako. Kwa maana kuna watu wengi sana misingi ya maisha yao ya baadae inaweza ikavurugwa kama hakuna mtu ataweka akiba kwa ajili ya msaada.

Unakuta saa nyingine nchi zinapata shida ya chakula ghafla wanatumia kile walivyokuwa nacho kama serikali yao ilivyoweka kinaisha, njaa inaendelea kama ilivyotokea Ethiopia wakati ule, usifikiri nchi yao haikuwa na akiba,lakini hakuna mtu aliyejua huo ukame utaendelea muda mrefu, hapa walisemeshwa miaka saba.

Mungu anaweza akakusemesha weka akiba ya kiwango fulani akijua utahitaji na inapowekwa ile akiba kikiisha inapelekwa taarifa kwenye nchi nyingine jamani eeh tumeishiwa chakula tunahitaji msaada. Zile nchi nyingine zinafungua maghala yao, zinapeleka chakula kwenye nchi zinazohitaji chakula na usifikiri wanatoa akiba zao bali wanatoa akiba walizoweka kwa ajili ya kuzisaidia  nchi zingine.

Ukitembelea na kuzunguka nchi zingine na kuzungumza nao habari za maendeleo utakuta nchi nyingi sana zina mifuko ya  maendeleo ya aina mbili. Kuna mifuko ya maendeleo kwa ajili ya nchi yao na mifuko ya maendeleo kwa ajili ya nchi zingine. Ambako ndio kunatokea international development assistance ndio maana ukienda kuomba msaada wanakupa tu. Usifikiri wanachukua ya kwao, ikiisha hiyo wanakuambia hatuna msaada, sio kwamba hawana hela, wanazo! Ila wametoa pesa nyingi sana kuliko walichopanga kutoa misaada duniani.

Ilipogundulika kuna shida duniani Umoja wa Mataifa (UN) ukaa chini na hizi nchi tajiri duniani na kuwawekea kiwango kwamba kila nchi iweke 20% kwa ajili ya maendeleo ya nchi changa na kila baada ya muda wanafuatiliwa na umoja wa mataifa kwamba kweli nchi hii imetoa na kuzidi, nchi hii haijatoa, hii imefikia nusu. Hiyo ipo kwenye ngazi ya kimataifa.

Lakini Mungu anazungunza kibiblia hapa kwenye ngazi ya kwetu wenyewe kwamba usiweke akiba kwa ajili yako tu peke yako. Kuna suala la watoto wajukuu, wageni  na majirani. Watu wengi sana wakitaka kusaidia wanasaidia kutoka kwenye mifuko yao ni kama vile unafukia shimo kwa kuchimba shimo.

Watu wanakufurahia kweli ulivyowasaidia lakini huku nyumbani kwako kumejaa mashimo. Unatengeneza lami kwa wenzako kwako kuna mashimo, wanatembea wanateleza wanamshukuru Mungu jinsi ulivyowasaidia lakini ghafla wewe unaanza kupita kwenye corrogation baada ya muda unaanza kuwakasirikia kwamba niliwasaidia lakini wao hawanisaidii.

Miaka ile ya 1990 wakati Mungu anatufundisha jambo hili wa nguvu, tulijiuliza na mke wangu, tuweke lengo, je kama hatutapata kipato chochote kwa miaka 2 na hatuna hela ya kututunza, itakuwaje? Tukatizama tukagundua hatuna, tukaanza kupiga mahesabu. 

Saa nyingine akina baba hatujui hayo mahesabu vizuri, kwa hiyo tukawa tunaulizana matumizi ya kila siku na gharama ya vitu mbali mbali tukaweka wastani wake kwa mwezi tukapiga mara 24 yaani miaka 2 tukapata kiwango, tulivyopata kile kiwango ndio likawa lengo letu kwamba hatutatulia mpaka tufikishe kiwango cha hela hii kiko benki na tusiiguse miaka 2 ikabidi tutengeneza account tofauti na tukawa tunadunduliza kidogo kidogo.

Ilituchukua miaka na tulifikia lengo na tukasogeza tena,  haya mambo tunayapata kwenye Biblia! Hawa waliambiwa miaka 7 kuna njaa lakini kuna watu wengi sana hapa ambao wana


ya kazi lakini akikosa kazi miezi hana ata akiba ya kumtunza. Anakazana kusema hakuna kazi hakuna kazi, sio kwamba hakuna kazi sema hakuna akiba. Kwa sababu ungekuwa na akiba usingepiga kelele lakini  unatazama kuna akiba halafu unasema pia kuna account ambayo ipo mbinguni unaotakiwa kunipa maarifa. 

Watu wengi wakisema hakuna ajira maana yake ajira ya kuajiriwa, Mungu hakukuleta duniani kuajiriwa. Mungu amekuleta duniani kufanya kazi, kwa hiyo kuna kazi ya kuajiriwa na ambayo sio ya kuajiriwa lakini wote hakuna aliyekuja duniani hana kitu cha kufanya. 

La sivyo usingeweza kupewa machine ya kumeng'enya chakula kwenye tumbo, kwa sababu hii machine inashughulika na chakula ili kiweze kufanya kazi, jaribu kula halafu usifanye kazi uone. Ile kwamba umeteremshwa mbinguni na machine ya chakula maana yake Mungu amekupangia kazi. Swala ni kwamba mahusiano yako na Mungu yamekaa mahali ambapo umebanwa kufikiria kwamba nimesoma kwa ajili ya hii kwa hiyo siwezi kufanya hii na unakwama.

Lakini unaweza ukajiajiri, kazi za kujiajiri hazijapungua zipo. Hatuombei mabaya lakini si kila nchi duniani ina serikali lakini utakuta wanaendelea wanaishi tu vizuri  hawana serikali yeyote watakayoinyoshea kidole. Lakini lazima watunze watoto, lazima watoto waende shule, lazima wavae. Serikali zina majukumu yake lakini ni hatari sana kwa mtu binafsi kuondoa wajibu wake juu yake na kukabidhi kwa mtu mwingine.

Biblia inazungumza kwa habari ya wana wa Lawi kupokea fungu la kumi kwa sababu Ibrahimu alitoa fungu la kumi Waebrania 7:5-10 kwa hiyo fungu la kumi kazi yake ni nini, Biblia inasema utainua misingi ya  vizazi vingi.

Kwa hiyo ukihesabu Ibrahim kama ni msingi wa kwanza ina maana Isaka ni msingi wa pili,Yakobo  ni msingi wa tatu na Lawi ni wa nne. Ukihesabu kuanzia Isaka basi Yakobo mbili na Lawi ni msingi wa tatu. Kibiblia kizazi kimoja kinahesabiwa kwa kipindi cha miaka 100. Utasema najuae? Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa kizazi cha nne kitarudi hapa ilipita miaka 400. Sasa ukigawa 400÷4=100. Kwa hesabu hizi ina maana kizazi ni miaka 100.

Ukijumlisha na kufika kwa Lawi ina maana kutoka Ibrahimu hadi Lawi ni miaka 400 yaani vizazi vinne. Hii miaka ni mingi sana kwa mbegu ya Ibrahimu kulindwa mbinguni. Mungu anakupa nafasi ya  vizazi vingi viwe na msingi wa kukanyagia maisha yao.

Mungu akikupa  nafasi nenda shule na uliza kama kuna mwanafunzi anayepata shida ya kulipiwa ada ya shule. Maana utakuwa unatengeneza msingi wa huyo mtu ambaye umemsaidia. Pia Biblia inasema utawekwa kwenye orodha ya watu ambao kazi yao ni kuinua misingi ya  vizazi vingi. Maana kuna siku atasema nisinge pata huu msaada nisingevuka hapa. Huyu uliyemsaidia yeye ataona ni msaada lakini kwako ni Sadaka.

Somo litaendelea. ..

Axact

Tanzania Worships

Haleluyah! Karibu katika ukurasa wa Tanzania Worships ambao ni maalumu kwa ajili ya kusambaza na kulihubiri Neno la Mungu anayeishi. je kuna maoni na ushauri unataka kuuutoa ili kuhakikisha ukurasa huu unawafikia waamini na wasioamini? basi usione shaka kuwasiliana nasi kwa njia ya mitandao ya kijamii

Post A Comment:

0 comments: