SEMINA YA NENO LA MUNGU~UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM
1 week ago

SEMINA YA NENO LA MUNGU~UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS KAWE - DAR ES SALAAM

Na Mwl. CHRISTOPHER MWAKASEGE.

SOMO: KUNENA KWA LUGHA KWA MUDA MREFU KUNAVYOSAIDIA UWEZE KUMWABUDU MUNGU
TAREHE  23 SEPTEMBA, 2019

SIKU YA PILI

KUPATA ANDROID APP YA HUDUMA, NAMBA ZA SADAKA, MAOMBI NA USHUHUDA, NAMNA YA KUPATA CDs & DVDs, KITABU CHA HONGERA KWA KUOKOKA, NAMNA YA KUSIKILIZA KWA ONLINE RADIO BONYEZA 
LINK HII 👉🏼http://bit.ly/2Xpccff

UTANGULIZI

LENGO LA SOMO
Kujifunza namna ya kumuabudu Mungu.
Kuweza kujua namna ya kushirikiana na upako wa kuabudu na kujazwa Roho Mtakatifu ili nguvu za Mungu au upako uweze kuongezeka ndani ya mtu.
Kutaka kuzidi kuimarisha uhusiano wetu na Mungu kupitia kwa Yesu Kristo


Na kitu ambacho Roho Mtakatifu ameninong’oneza pamoja na kwamba zipo nguvu zake na zitafanya vitu vingi kupitia somo hili lakini kuna msisitizo maalum kutoka mbinguni kuachilia upako wa kuabudu juu ya kila mtu ambaye atataka kuona anamuabudu Mungu jinsi inavyompendeza Mungu.

Na leo nitafundisha kwa mtindo/mfumo wa kujibu maswali. kwa leo hayapo maswali mengi sana yapo kama maswali matatu hivi na majibu yake yana vitu vizito ndani yake;

SWALI LA KWANZA
1. KUABUDU NI NINI?

Kuabudu ni kumwambia na kumuonyesha Mungu yeye ni nani kwako na wewe ni nani kwake.

SWALI LA PILI
2. KUABUDU NI KUFANYA NINI?

Kuabudu ni kumtafuta Mungu kwa nia ya kutaka kujenga mahusiano naye binafsi kati ya wewe na yeye.

Kumbuka tulipotoka na tunapoelekea maana hii ni maana mojawapo na tutaendelea kuangalia maana moja baada ya nyingine mpaka Mungu atakapotupa nafasi ya kuziangalia zote 5, ikimpendeza halafu utazikusanya zote 5 na ndipo utakapoelewa kwanini upako wa kuabudu una nguvu kuliko upako mwingine wowote.

Mathayo 15:8-9
“Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.”

Mathayo 18:11-13
“[Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa kilichopotea.] Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea.”

Sasa inapofika kwenye kumwabudu/kumuheshimu Mungu haijalishi njia unayoitumia unapoenda kumuabudu Mungu, anachotafuta kwanza ni moyo wako si maneno unayomwambia ila moyo uliokuja na hayo maneno, si sadaka unayompa bali moyo uliokuja na hiyo sadaka.

Kati ya jambo mojawapo ambalo si watu wengi sana wamelitazama ni kwamba dhambi ilipokuja duniani haikuleta tu hasara kwetu bali ilileta pia hasara kwa Mungu. Kwa sababu Mungu alipoteza kitu na sisi tulipoteza kitu. Maana Mungu alipokuwa akimuumba mtu alimuumba kwa mfano wake na kwa sura yake, roho ya mwanadamu iliumbwa kwa ajabu na thamani sana na kile kilichomfanya Yesu kuja duniani ni kuja kukiokoa kilichopotea. Biblia ya kiingereza kilichopotea inazungumza juu ya kile ambacho kime “lost” sasa hili neno lost ni kile kilichopoteza njia ya kurudi mahali ambapo kinatakiwa kurudi/kukaa.

Sasa mwanadamu alipoteza moyo wa Mungu na Mungu alipoteza moyo wa mwanadamu. Na ukitaka kuunganisha haya maneno soma kile kitabu cha Yohana

Yohana 4:23-24         
“Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

Mungu anazungumza na kusema hawa wananiabudu bure maana yeye hapati faida na wao hawapati faida. Maana unapoabudu anatafuta moyo wako kwanza, anatafuta kurudisha mahusiano yale ya mwanzoni yaliyokuwepo ambayo alikuwa ameyakusudia na dhambi ndiyo iliyotuvurugia.

Kwa hiyo Mungu anatafuta kwanza moyo wa mtu kwa sababu moyo wa mtu uliumbwa upate kumwabudu Mungu. Maana mwanzoni kabla ya maombi kulikuwa na kuabudu na maombi hayakuwa maombi bali ilikuwa ni ushirika (fellowship). Watu walikuwa hawaendi kwa Mungu kutafuta vitu bali walikuwa wakienda kwa Mungu kumuabudu. Na katika kumuabudu walikuwa wanajikuta wana kila kitu wanachokihitaji.

Kwa lugha nyingine kuabudu ni moyo wako unaenda mbele za Bwana au roho yako inautafuta moyo wa Mungu ili muwe na mahusiano binafsi.

Na Mungu anapokuja mahali unapoabudu au anapoachilia roho ya ibada ndani yako, anapokusukuma na kitu cha kuabudu ndani yako utasikia hamu ya kutaka kumjua. Kwa sababu kitu anacho tafuta ni kuja kupokea moyo wako. Wewe unaachilia moyo wako unamtafuta Mungu aliye hai. Lakini kwa sababu umepotea huna namna ambavyo unaweza kumtafuta na kitu Mungu alichofanya kwa neema yake na kwa rehema zake akaamua kukutafuta. Na katika kukutafuta kwake akaja na maagano tofauti tofauti mpaka lilipotokea agano jipya maana agano la kale mambo yalikuwa yakifanyika kwa kivuli alikuwa halisi.

Katika agano jipya Damu ya Yesu Biblia inaweka wazi kabisa ya kwamba inawakamilisha wale wakaribiao wapate kumwabudu, kwa sababu sadaka ya damu ya mafaali haikuweza kabisa kumkamilisha yoyote yule aliyeenda mbele za Mungu kumuabudu. Pamoja na kwamba damu hiyo haikuwa imefikia kumweka mtu katika ngazi hiyo bado Mungu aliheshimu hilo agano na akawa anapokea zile ibada kwa namna ambavyo hakuruhusu kila mtu aweze kumkaribia kwa kiwango ambacho angetaka, kwa hiyo aliruhusu tu kuhani mkuu mara moja kwa mwaka angalau aingie patakatifu pa patakatifu.

Kwa sasa Biblia inasema tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu (watu wengi sana hufikiria ni maombi) lakini Mungu alipokuwa akifungua mlango wa patakatifu alikuwa hawazii maombi, alikuwa anawazia mahusiano yake na mtu binafsi aingie humo na kupata nafasi ya kumuabudu.

Yohana 17:1-3
Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.

Uzima wa milele maana yake ni Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.
Kwa hiyo kazi ya uzima wa milele ni kukujulisha Mungu ni nani na Yesu ni nani.
Kazi ya uzima wa milele si tu kukupa wokovu bali cha kwanza Kukujulisha kutengeneza mahusiano yako na Mungu umjue Yeye ni nani. Kwa hiyo uzima wa milele ni zaidi ya kuokoka, kwa maana kuokoka ni matokeo ya uzima wa milele kuingia kwako.
KUABUDU ni:
(i) Kumwambia na kumuonyesha Mungu Yeye ni nani kwako. 
(ii) Kumtafuta Mungu kwa nia na lengo la kutengeneza na kuimarisha mahusiano yako na Yeye. Mungu anapokuja kwenye ibada lengo lake la kwanza ni kutafuta mioyo inayomtafuta ili ajijulishe kwao.  Kwa hiyo watu wanavyoongozwa sala ya toba ni hatua muhimu sana ya kumuabudu Mungu. Ni sehemu muhimu ya ibada.
Ukienda kanisani Biblia inasema kunakuwepo na mambo ya ibada na kuabudu.  Kunaweza kukawepo mambo ya ibada bila ya kuabudu. Na kuabudu ndipo kunakotakiwa kuzae ibada, na kama watu wanafanya mambo ya ibada bila kuabudu Biblia inasema wanaabudu bure ambapo siyo halisi.  Mtu anakuja kwenye ibada halafu Mungu hapati faida yoyote wala Yeye hapati faida yoyote lakini wamefanya ibada.
Kama uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma, kitu gani kinachowafanya watu kanisani waanze ibada na kumaliza pasipo kuwapa watu nafasi ya kutubu na kuokoka? Nafasi ya kuongozwa sala ya toba na kuokoka wakati wa ibada ni kitu kimojawapo cha msingi sana ambacho Mungu anakitafuta.
Ibada ni sehemu muhimu ya kujenga na kutengeneza mahusiano yako na Mungu.  Kumbuka unaweza ukatubu lakini usijenge mahusiano, mfano mnaweza kugombana na mtu mkatafuta mtu wa kuwapatanisha na bado mkashindwa kurudisha mahusiano.  Mfano unagombana na Mungu unaenda ibadani na mpatanishi kati yako na Mungu ni mhubiri, utakuta Mungu anasema nimemsamehe na wewe unasema nimemkasirikia Mungu lakini nimemsamehe, lakini mkaondoka hamuongei.  Kila ukimuuliza mbona huonekani kanisani, unasema mimi Mungu nimemsamehe, na Mungu akiulizwa mbona humtembelei? anasema mimi nimemsamehe.
Musa alipoambiwa unaweza ukaenda lakini mimi siendi aligoma na kusema Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa - we are not moving- kwa sababu suala hapa siyo ahadi, hatukuja kutafuta uhusiano kwa sababu ya kutupeleka Kanaani, wala alikuwa hatafuti msaada wa Mungu safarini bali uwepo wake maishani. Mungu alimuahidi kuwapa malaika kuwapigania safari nzima lakini Musa aligoma.
Kutoka 33:12-19‬
Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako. Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la BWANA mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.
Umewahi kujiuliza kwa nini wakati wa mikutano ya kiroho kama hii au kanisani, ikifika saa ya kuokoka waliookoka wanakuwa wa kwanza kuondoka?  Saa Mungu anafurahia moyo wa aliyepotea unarudi, ndiyo saa ambayo waliookoka wanaondoka.  Lazima kuna shida mahali au hujajua thamani ya Yesu kufa msalabani? Hujajua heshima ambavyo Mungu anapata mbinguni mtu mmoja anapookoka?
Luka 15:4-7
Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

Towashi aliyekuwa Mkushi alisikia habari za Yesu kama iliyoandikwa kwenye Yohana 17:3 Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.  akafunga safari akaenda Yerusalemu kuabudu.
Matendo 8:25-39
Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria. Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? [ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

Yohana 4:23-24
Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Lile neno roho ni herufi ndogo maana yake roho(spirit) yake. 
Mathayo 15:8
“Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.‭‭

Na ukienda ile Mathayo 15:8-9 anaposema wananiabudu bure mioyo yao iko mbali nami .Kule ndani amejumuisha roho na nafsi ya mtu. Na hivyo vitu anavizungumza kwa uzito wake kwamba katika kipindi hiki ni lazima tumuabudu katika roho na ni lazima roho yako ihusike, lakini akaweka na kitu kingine,  katika roho na kweli. Kweli inatafsiri mbili pale, na tafsiri ya kwanza ambayo watu wengi wanaiona ni ile iliyopo kwenye kitabu cha Yohana watakase na ile kweli na neno lako ndio kweli. Kwa hiyo inajulikana umuabudu Mungu katika roho na kusimamia kwenye neno. Sasa kama huna neno hujalelewa kwenye jamii ya kikristo, lakini ghafla ndani yako au umesikia watu wakisema juu ya huyu Mungu na huna kitabu hata kimoja, sio kila mtu alikuwa na Biblia kama tulizonazo leo, sio kila mtu alipata nafasi ya kupata kitabu cha nabii Isaya. Sina uhakika huyu ndugu alikipata hiki kitabu wakati anaenda au alikinunua Yerusalem    wakati anarudi.
Maana nyingine ya kweli maana yake halisi (genuine), moyo usiokuwa na unafiki, Mungu anakutaka uende ulivyo. Biblia inaposema Zaburi 96:9 kumwabudu Mungu katika uzuri wa utakatifu , watu wanafikiri watu ambao hawajaokoka hawawezi kumuabudu Mungu, inategemea unachukua maana ipi ndani ya kuabudu maana utawafungia nje wengine. Lakini ukichukua hii ya kwanza ambayo naenda nayo leo huna haja ya kumfungia nje ambaye hajaokoka kwenda kumuabudu Mungu.
Kwa sababu huyu ndugu alikuwa hajaokoka alienda Yerusalem kuabudu, alikuwa haendi kwenye mambo ya ibada, hana interest(nia) na ibada lakini ana interest (nia) ya kumjua huyu Mungu, na maandiko yanasema ibada iliisha hajakutanishwa na huyu Mungu na kiu iko pale pale akaanza kusoma kitabu cha nabii Isaya kwa sauti na akaanza kujiuliza mbona huyu Mungu wanayesema anapatikana kwenye ibada zao mbona sijaonana naye? Nimekuta tu ibada inaendelea lakini huyu Mungu wanayesema wamekuja kumuabudu mbona sijaonana naye!
Filipo alikuwa katikati ya uamsho mkubwa sana kule Samaria, kulikuwa na miujiza ya kila namna kule ikifanyika na mji ulikuwa na furaha kubwa, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo achana na huo mkutano nenda ile njia ya kuelekea Gaza, wakati mwingine kama watumishi wa Mungu tungesema kama Mungu ameniambia niende mahali pengine, huwa tunahisi kutakuwa na mkutano mwingine mkubwa zaidi ya huu, akajikuta anaenda na kukutana na mtu moja yuko kwenye gari na akalisogelea lile gari, sasa angalia Filipo alipouliza yamekuetea haya unayoyasoma akajibu nitawezaje kuelewa mtu asiponiongoza? 
Kwa lugha nyingine nimekaa kwenye ibada hakuna aliyeniongoza, hakuna aliyenielewesha, na inawezekanaje nimekaa kwenye ibada muda wote huu mimi sikuja kwenye ibada nimekuja kwa ajili ya kumtafuta huyu Mungu anayeabudiwa hapa, najaribu kufikiri huyu mtu alimwambia Filipo kuna watu walikuwa wanaongoza ibada lakini hawakuniongoza kwa Yesu.
Jibu la huyu mtu anasema sina mtu wa kuniongoza, hakusema hakukuwa na mtu wa kuongoza ibada nataka mtu atayeniongoza mimi nimjue huyu Mungu na sijui hata nakutanaje na yeye.  Sijui nampataje moyoni mwangu, nimekuja na moyo wangu kutoka Kushi na narudi nao hivi hivi sina mtu wa kuniongoza ili nimkabidhi Mungu. Yule ndugu alimsomea Filipo mistari, inawezekana ndio walioisoma kwenye ibada na angalia jinsi Filipo alivyokuwa amejawa na nguvu za Roho Mtakatifu akaanza kumueleza habari za Yesu kutoka kwenye mistari ile ile! Mpaka huyo ndugu akaamua kuokoka akapokea uzima wa milele ndani yake akamjua Yesu aliyetumwa, akamjua Mungu wa kweli na wapekee. Baada ya pale aliondoka akienda kwa Furaha.
Unafikiri kwanini Filipo aliachishwa ule mkutano? Ili Mungu atuonyeshe umuhimu wa kuwapa watu nafasi ya kumjua Mungu katika ibada! Kuna makanisa mengine yanafikiri katikati ya ibada hakuna wasiookoka, wakifikiri watu wote wameokoka kwa sababu wakisema Bwana asifiwe kila mtu anasema Ameen! Na kwa sababu hiyo hata Roho Mtakatifu akiwapa nafasi ya kuitisha watu kuokoka wanasema si nitaonekaka kanisa langu lina watu ambao hawajaokoka! Nani aliyekuambia msalaba ni wa wasafi, kwa sababu kama unauinua msalaba na Yesu aliyekufa atawavuta watu wote waje kwake. Ufalme wa Mungu ni kama Juya(wavu wa kuvulia)  utabeba samaki pamoja na makopo.
USHUHUDA
Nilienda kwenye kanisa moja baada ya kuitisha watu kuokoka kila mtu alishangaa kuwa niliwezaje kuitisha watu kuokoka kwenye kanisa la waliokoka. Baba mmoja akasema naomba kushuhudia, nikamsikiliza kikampa mike, akasema hivi ‘hili ni kanisa langu la tatu nahama nakimbia wokovu, akasema nilikuwa kanisa moja wokovu ulivyoingia nikahama, nikaenda kanisa lingine la pili, wokovu ulivyoingia nikahama nikatafuta kanisa ambalo watu wote wameokoka nijifiche huko, akasema sijawahi kusikia hata siku moja mchungaji akiita watu kuokoka. Leo umezungumza kitu kigumu nimeshindwa kukimbia, unafikiri mchungaji wake aliwaza nini!

USHUHUDA
Nilienda mkoa mwingine kwenye kanisa moja, wakati ninamalizia kufundisha Roho Mtakatifu akaniambia, mimi sina wajukuu nina watoto, nikasema unamaanisha nini? Akasema kuna watoto wa waliookoka wamejificha kwenye wokovu wa wazazi wao hawajawahi kuokoka hata siku moja. Kwa hiyo na mimi nikaeleza hivyo hivyo, wewe ambaye upo hapa kanisani unajua hujawahi kumkiri Yesu kwa kinywa chako binafsi, wokovu ulionao ni kwa sababu wazazi wako wameokoka njoo mbele umpate Yesu wako binafsi, wakatoka wengi sana.
USHUHUDA
Tulikuwa kwenye semina mkoa mmoja namna hii, na nguvu za Mungu zilishuka na watu wamejaa hapa mbele kila mahali na mahali pa kupita hakuna, nilikuwa nawaombea waombaji nguvu za Mungu nikaona, mke wangu akaniambia njoo, akaniambia unaona huyu amelewa na saa hiyo aliponionyesha walikuwa wameshamwombea na sala ya toba, nikauliza ametokea wapi wakasema sisi hatujui na yeye tumemuuliza amesema hajui.
Kwa hiyo fahamu hili nililokuonesha ili uweze kujua. Lakini ukirudi tena kwa Filipo. 
Ile Filipo alipoondolewa kule kwenye mkutano inatuonyesha kwamba kipaumbele cha Mungu ni kuabudu sio maombi, maombi yanakuja kama matokeo ya kuabudu. Huku alikuwa akikazana kuhubiri na kufanya maombi kwa wenye shida mbalimbali lakini kulikuwa na mtu mmoja anataka kuabudu, amekuja kanisani kutafuta kuabudu hakuja kutafuta maombi, na hakupata alichohitaji kwa sababu kanisani walikuwa wanafanya maombi na akatafuta kitu cha kuabudu hakupata, Mungu akamtoa muhubiri katikati ya maombi akampeleka kwa mtu mmoja anayetafuta kumjua Yesu. 
Sikuambii maombi ni mabaya ila vipaumbele (priorities) vya Mungu, maombi yana sehemu yake, hii inamaanisha kwamba Mungu anajali mahusiano tuliyonayo na yeye, kuliko vitu anavyotupa ambavyo hata saa nyingine havitutengenezei mahusiano yeyote na Mungu. 
Unaweza ukawa na vitu vya Mungu bila kuwa na mahusiano na Mungu na Mungu hakukatalii atakupa. Mnamfahamu yule mtumishi Akida aliyemwambia Yesu ana mgonjwa nyumbani alafu alipopeleka taarifa Yesu akaamua kwenda, Yule Akida akamzuia njiani, akasema nakufahamu unamamlaka makubwa sana huhitaji kwenda nyumbani sema neno tu, sasa Yesu anasema sijawahi kuona imani kubwa namna hii, na iwe kwako kama ulivyosema na yule jamaa akaondoka na alipofika nyumbani mgonjwa amepona, ukisoma kwanza utaanza kufikiri kwa namna hii huyu jamaa alikuwa na ujasiri gani wa kumkataa Yesu asiende nyumbani kwake. Unamtaka Yesu nyumbani kwako au unataka uponyaji wake nyumbani kwako. Kitu gani kinakufanya uupokee uponyaji wake alafu usimpokee yeye.
SWALI LA TATU
3. KWANINI KIU YA KUTAKA KUMJUA MUNGU ZAIDI INAPUNGUA NA  INAPOTEA BAADA YA MTU KUOKOKA? NA KWANINI PIA KIU YA KUTAKA WATU WENGINE WAMJUE MUNGU ULIEMPATA INAPUNGUA?

Mathayo 15:1‭-‬9
Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe. Bali ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, Cho chote kikupasacho kusaidiwa na mimi ni wakfu, basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu. Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,   Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.  Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.
Na 
Mathayo. 22:29
Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.
Kwa wale wazee wa zamani, Dalili ya kwamba mtu ameokoka ni kiu ya kutaka watu wengine wamjue Mungu ulienae inakuwa kubwa lakini baada ya muda inapotea, na watu hawajajua kuwa hiyo ni sehemu ya ibada na upako wa kuabudu, unakaa juu yako tukichukua kuabudu kama kumwambia Mungu yeye ni nani kwako. Kwa mfano akiimba wimbo wa "Cha kutumaini sina ila Damu yake Yesu" unamtukuza Yesu ila ukiimba "Cha kutumaini sina ila Damu yako Yesu" unamwabudu Yesu kwa sababu kuabudu unamwambia Mungu Mungu lakini kutukuza unawaambia watu habari za Mungu sasa kitu gani kinamfanya mtu anapookoka anakuwa bize kwenye mikutano mingi sio kitu kingine bali ni kiu ya kutaka kumjua Mungu.
Lakini kitu gani kinafanya hiyo kiu ipotee baada ya muda? Yesu anasema Ni kwa sababu hatujui neno wala uweza wa Mungu na Mapokeo yanatangua neno la Mungu. Ukiona mtu amepoa ndani yake na anasema yeye sio mhubiri kwa hiyo hawezi kuwaleta watu kwa Yesu. Biblia inasema "kila alie nae Mwana ndani anao ushuhuda" atakaeweza kujitetea ni yule asie na mwana ndani ambaye hajaokoka. Maana kila alieokoka anao ushuhuda kwa hiyo anao uwezo wa kumshuhudia mtu Mwingine kitu Yesu alichomfanyia ndani. Kwa hiyo huwezi kujitetea eti kwa sababu wewe sio mhubiri.
Inawezekana umepita mahali ambapo pameondoa kipaumbele chako cha mahusiano yako na Mungu na kuweka kipaumbele cha mahusiano yako na mahali unaposali. Unaokoka na unaenda kuabudu mahali ambapo hawakupi mafundisho ya kutaka umjue Yesu vizuri, lakini  wanakupa mafundisho ya kutaka ulijue kanisa lao vizuri, sikuambii ni vibaya kufundishwa mapokeo ya Kanisa lao kwa sababu utaabuduje bila kufahamu wenzako wanafanyaje hapo, lakini ninachozungumzia hapa ni kipaumbele. Kwa sababu kama mapokeo yataharibu na kupoteza ile kiu uliyoipata wakati unaokoka. Ndio maana nakuambia soma Biblia mwenyewe.  Unapookoka kunakuwa na Moto ndani yako na Mchungaji hawezi kuuchochea wala jirani yako, kama umeokoka tayari umeshakuwa na mahusiano yako na Mungu kwa hiyo ni jukumu lako kuuchochea huo moto, kwa hiyo usisingizie unaposali ndio pamekufanya upoe ni wewe mwenyewe ndio umepoa kwa sababu ulitegemea Mwingine auchochee.
USHUHUDA
Kuna wakati nilienda Uingereza nikakaribishwa kwenye kanisa moja, Nilizunguka robo tatu ya ile nchi. Kuna siku alinisemesha kitu kigumu sana akasema "Mwakasege zamani tulikuwa tunajenga mahusiano yetu na kanisa mpaka tulipojua tunatakiwa kujenga mahusiano yetu na Bwana wa kanisa kwanza ndio atusaidie kujenga mahusiano na Kanisa lake." Nilimtazama yule jamaa maana sikutegemea alichosema.
Wengine wakishaona namna hiyo wanahama kwenye hilo kanisa  maana wao wanafikiri kuhama ndio Dawa. Lakini hata ukienda huko kumbuka kuwa hakuna kanisa lolote ambalo halitakufundisha taratibu za ibada zao. Hicho ni kitu sahihi kabisa lakini mambo ya ibada ya wewe na Mungu ni suala lako. Kwa hiyo unatakiwa kulilinda na kulitunza sana. Maana unaweza kwenda mahali pengine na ukakutana na mtu aliyeokoka na akakufundisha kujenga mahusiano na Filipo wako badala ya Yesu ambaye Filipo alikujulisha kwake.
Je wewe unafikiri kwanini Filipo alinyakuliwa? Hii ni kwa sababu yule jamaa asije akajenga mahusiano na Filipo badala ya kujenga mahusiano na Yesu. Pia inawezekana kuna sababu zingine ambazo zingemfanya Filipo apelekwe mahali pengine, lakini Mungu alifanya vile ili kuwafundisha watu wengine wasijenge mahusiano na watu waliowaongoza kuokoka badala ya kujenga mahusiano na Yesu waliyempokea baada ya kuokoka. Kwa maana hiyo wanajikuta baada ya muda wanaanza kupoa.
Kujenga naye mahusiano sio vibaya maana huyo ni baba yako au mzazi wako wa kiroho hayo mahusiano yako yatakuwepo. Lakini tambua kuwa baada ya kuokoka Yesu lazima apewe nafasi ya kwanza. Kitu kinachowafanya watu wapoe ni kuwa wanapofika saa ya ibada wanakuwa na msisitizo wa Ibada badala ya kuwa na msisitizo wa kuabudu wakati wanafanya ibada.
Kwa mfano, Mara nyingi sana watu wakiombea nguvu za Mungu zije kwenye ibada, huwa hawaombi nguvu za Mungu zije kwenye ibada kama ilivyo katika Wafilipi 3:3. Inasema sisi ni watohara tumuabuduo Mungu kwa Roho (By the Holy Spirit) kwa msaada wa Roho Mtakatifu . Kwa hiyo ukiombea ibada ili nguvu za Mungu zije kazi yake ni ili ziwasaidie watu wapate msaada wa kumuabudu Mungu.
Watu wanaweza kumuombea mhubiri  aweze kuhubiri tu lakini huwa hawamuombei ili pate ujasiri wa kuita watu kuokoka, kwa sababu wao wanafikiri ni kitu chepesi kuita watu kuokoka. Maana sio kitu chepesi kwa mhubiri kwenda kuhubiri kwenye kanisa ambalo sio la kwake na Roho Mtakatifu akamwambia itisha watu kuokoka, ujue kabisa kama hana ujasiri itakuwa changamoto sana kwake kufanya hivyo. Kwa hiyo hakikisha mnamuombea mhubiri awe na ujasiri wa kuhubiri na kuita watu waje kwa Yesu.  Kwa hiyo haijalishi unahubiri au kufundisha neno la Mungu lina nguvu ya kuokoa kwa hiyo usijaribu kusema wewe sio, mhubiri unafundisha tu, hiyo sio sababu ya kutoita watu kuokoka.
Kwa sababu Mungu ndiye anayetaka watu waokoke sio wewe. Hata kama ni mtu mmoja anataka kuokoka Mungu atahakikisha huyo mtu anaokoka hata kwa kumtuma Filipo aende akamweleze habari za Yesu wakati anarudi nyumbani kwake. Maana anajua  hiyo nafasi ni ya kwake  na anastahili kupewa nafasi ya kumjua Mungu.
USHUHUDA
Nilipokuwa naenda kwenye misiba nilikuwa napewa nafasi ya kuhubiri  mara nyingi huwa sipendi kuhubiri kwenye misiba. Kwa hiyo kuna wakati nilikuwa najikaza kukataa wakati nikipewa nafasi ya kuhubiri lakini mahali pengi niliweza.  Sasa haijalishi nilivyoanza kuhubiri lakini kila ikifika mwisho Roho Mtakatifu ataniambia kuwa niite watu kuokoka. Kwa hiyo haijalishi kuna jeneza hapo karibu lakini Roho Mtakatifu akisema ita watu kuokoka huwa nasimamisha kila kitu na kutii wito wa Roho Mtakatifu.
Kwa sababu ninaelewa kitu anachotafuta maana kuna watu wengine wanakuwa na utayari zaidi wakati wa msiba maana ndio wakati ambao wanafungua masikio ya ndani na nje. Maana hata ukiwaambia Yesu karibu anarudi tazama juu huwa wanatazama kabisa. Kwa hiyo waombaji wahakikishe kuwa wanawaombea wahubiri  ili wapate nafasi  na ujasiri wa  kuita watu kuokoka.  Maana hata kama taratibu za kanisa hilo hawaruhusu Mungu atampa mhubiri hekima katikati ya mitego ili aweze kuita watu kuokoka.
Maana akiona kama taratibu zinambana zaidi basi anaweza sema kwa yule ambaye ataona neno limemogusa zaidi basi anaweza niona hapo nje ili apate kuokoka na kumjua Yesu binafsi. Baada ya muda utaona watu wanakuja kusema mtumishi neno lako limenigusa kwa hiyo nataka kuokoka. Kwa hiyo unatakiwa kuombe nguvu za Mungu katika kuabudu maana nguvu za Mungu zikija huwa “zina sub seed kila objections na impediments”. Kwa hiyo kila kitu ambacho kinazuia usipate kitu ambacho kilimfanya Mungu amtume mtoto wake Duniani.
Kwa hiyo unapoombea nguvu za Mungu katika ibada sio tu uombe ili watu waongeze vizuri taratibu za ibada bali waweze kuabudu. Kubudu sio kuimba nyimbo za kuabudu, maana haijalishi ya ibada inaanzia wapi lakini viongozi wanaongoza ibada lazima wawe na nia ya kutaka watu wanaoingia pale kanisani wae na lengo la kutaka kumjua Mungu. Na ndio maana Mungu huwa anaweka waombaji ili waweze kuomba kwa ajili yao.
Baada ya muda utaona watu wanapoteza nguvu na baada ya muda wataona ile kiu inapotea. Nehemia 8:10 inasema furaha ya Bwana ndio nguvu zetu. Maana furaha ya Mungu ni pale anapoona mwenye dhambi mmoja akitubu. Kwa hiyo anapokosa ile furaha yake ya kupata moyo wa mtu huwa anaondoka hana furaha. 
Kuna wakati mwingine Mungu hafurahi kwa sababu anakuwa amekosa moyo wa mtu, maana amekuja kwenye ibada kwa ajili ya kumuimbia na kumpa sadaka na hujampa moyo wako. Mungu akikosa furaha utasikia ndani yako  maana huwa anakaa ndani yako. Daudi aliimba kuwa naomba nirejeshee furaha ya wokovu maana yake nirejeshee furaha ya kukujua Mungu maana imepotea ndani yangu.
Zaburi 51:11-13
Usinitenge na uso wako, Wala Roho yako Mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. 
Kwa hiyo uzito wa kuwashuhudia watu wengine ni kwa sababu furaha yako ya wokovu  imepotea, kwa sababu nguvu za Mungu zimepungua ndani yako. Kwa sababu furaha ya Mungu ndio nguvu yetu. Kwa hiyo Mungu akiacha kufurahi nguvu huwa zinapungua ndani yako. Kama kilichomfanya Mungu asikitike ndani yako ni kwa sababu hujawapeleka watu kwa Yesu kuna mawili ni aidha moyo wako uko mbali na Yesu au huoni umuhimu wa kuwapeleka watu kwa Yesu.
Ukishaona huoni umuhimu wa namna hiyo utapoteza muda wa kukaa na Mungu kwenye Ibada. Ndio maana watu wakienda kwenye ibada huwa wanachunga sana muda, ambao wanakaa kwenye ibada kuliko kile wanachopata kwenye  hizo ibada. Muda una sehemu yake lakini inatakiwa utoke kwenye ibada una kiu na unataka hata wakisema kuna ibada nyingine aweze kurudi tena. Hii ndio maana unakuta mtu kwa siku anaenda ibada hata mara tatu, hii ni kwa sababu Mungu anajibu kiu ya moyo wake japo yeye anafikiri kama anaweza kuipata mahali popote lakini anahitaji kujua kuwa kiu iliyopo ndani yake ni Mungu ambaye anaihitaji  na ndio maana alisema kila aliye na kiu na aje kwangu.
Ikifika mahali huna hiyo kiu nenda tena kwa Bwana omba toba ili Mungu akurejeshe furaha ya wokovu, ili  kiu ya kutaka kuwahubiri watu habari njema ya wokovu irudi tena uweze kuwahubiri habari za Yesu. Ukishatubu unaomba Mungu akujaze tena nguvu zake maana biblia inasema nanyi mtajaa nguvu na nanyi mtakuwa mashahidi maana yake mtakuwa na uwezo wa kushuhudia. Maana huwezi kushuhudia peke yako bila msaada wa Roho Mtakatifu. Ndio maana Biblia inasema wote wakajazwa nguvu na wakaanza kusema kwa lugha mpya kama Roho alivyowajalia kusema. Kwa hiyo hata kama kesho na kesho kutwa nguvu zikiisha unaendelea kunena kwa lugha mpaka ile furaha irudi tena. Jaribu kunena kwa saa moja utaona mabadiliko ndani yako maana utasikia inaingia kiu ndani yako ya kutaka kumjua Mungu.

Wimbo wa nafsi yangu ya kutamani… roho yangu yaona kiu….

Mwisho wa Day 2…… Barikiwa sana…..
Axact

Tanzania Worships

Haleluyah! Karibu katika ukurasa wa Tanzania Worships ambao ni maalumu kwa ajili ya kusambaza na kulihubiri Neno la Mungu anayeishi. je kuna maoni na ushauri unataka kuuutoa ili kuhakikisha ukurasa huu unawafikia waamini na wasioamini? basi usione shaka kuwasiliana nasi kwa njia ya mitandao ya kijamii

Post A Comment:

0 comments: