*NI NINI MAANA YA KUIFIA DHAMBI?*

 Mwl Raphael Mtui(0762 731869)

Warumi sura ya sita imeendelea kutueleza kwa undani jinsi ambavyo Yesu alituokoa, maana tulijiuliza sana alituokoaje, au tunaokokaje kutoka kwenye dhambi. Ni katika sura hii Biblia imetuhakikishia kuwa *dhambi haitatutawala tena.*(Mstari wa 14).

 Lakini kuna fumbo lingine mwanzoni mwa sura hii ambalo limetumia maneno mazito kabisa yanayoeleza jinsi tumeokoka kutoka dhambini

Tumeambiwa kwamba TULIIFIA DHAMBI, NA TUJIHESABU SISI NI WAFU KWA DHAMBI. Warumia 6:2 *.....Sisi TULIOIFIA DHAMBI tutaishije tena katika dhambi?* Warumi 6:11 *Vivyo hivyo ninyi nanyi JIHESABUNI KUWA WAFU KWA DHAMBI na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.* Maswali ni mengi kwamba tulikufaje! Mbona hatukuwahi kufa? Tumeifiaje dhambi?

 Ni nini hicho kilikufa, na kilikufaje? Jibu tunalipata katika mstari wa sita: Warumi 6:6 *mkijua neno hili, ya kuwa UTU WETU WA KALE ULISULIBISHWA PAMOJA NAYE, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;*

 Ahaa. Kumbe kilichosulibiwa na kuuawa ni utu wetu wa kale. Sasa, utu wa kale ni nini? Wasiliana nasi nitakutumia somo letu liitwalo UTU WA KALE NI NINI? Kwa kifupi, utu wa kale ni ile hali ya udhambi tuliyoirithi kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva. Tangu walipotenda dhambi, walituambukiza hali ya uharibifu mkubwa sana, iliyopelekea tuwe katika hali ya dhambi tu, hata kama tunajitahidi kutenda mema, bado tulistahili hukumu. Warumi 5:14 *walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja.* *_Kama hujaokoka, lakini unajitahidi sana kuwa mtenda mema, haitakusaidia, bado unahitaji Mwokozi wa kuua/kusulibisha utu wako wa kale ndani yako, ili uzaliwe mara ya pili na kuwa kiumbe kipya, yaani utu wa kale utolewe kabisa ndani yako na kuvaa utu mpya._* Kama ukiwa mtenda mema huku unakataa kuokoka, ni sawa na mchungwa unakataa kuitwa mchungwa kisa hauna matunda(machungwa).

 Yaani, ni mtu mwenye utu wa kale ndani yake, ila anajitahidi kutenda mema huku nje, hivyo anataka asiitwe mchungwa, yaani mdhambi. Mradi wewe ni mwanadamu, ulizaliwa na utu wa kale, na hivyo kuwa mdhambi moja kwa moja, na hivyo UNAHITAJI MWOKOZI TU. Bila hivyo, ukitaaa kuokoka, yaani kumwamini Yesu kama Mwokozi na kutubu, kisha kubatizwa ki-Biblia, lakini ukawa mtenda mema, bado utakuwa ni mfu kwa Mungu ambaye unajitahidi kutenda mambo yaliyo hai.

 UJUMBE MKUU WA WOKOVU HUWA HAUENDI MOJA KWA MOJA KUWAAMBIA WATU WATENDE MEMA KABLA HAWAJAOKOKA. INA MAANA KUSINGEKUWA NA NENO *TUBUNI* KWENYE BIBLIA. WALA KUSINGEKUWA NA NENO *MBATIZWE* KWENYE BIBLIA. BIBLIA ISINGEAGIZA TOBA WALA UBATIZO, INGEAGIZA TU WATU WATENDE MEMA TU MOJA KWA MOJA, NA INGEMAANISHA YESU HAKUJA DUNIANI KUTUOKOA, BALI NI SISI TUTAJIOKOA KWA MATENDO YETU MEMA BILA TOBA WALA UBATIZO, YAANI BILA KUHITAJI MWOKOZI. MAHUBIRI YOTE YA YESU NA MITUME YALIANZIA HAPA: TUBUNI, MBATIZWE, NDIO UWE MWANZO WA KUANZA KUTENDA MATENDO MEMA YAPASAYO TOBA, ILI YAWE NA MAANA. KWA MAANA MATENDO MEMA BILA WOKOVU HAYANA MAANA.

 Tuache hayo; Si unajua kabla hatujaokoka tunaitwa wafu kwa Mungu maana tunakuwa tumetengana naye? Tunakuwa wafu kwa haki, na tunakuwa hai kwa dhambi. (Soma Waefeso 2:1,5) Lakini mambo yanakuwa vice versa mara tunapookoka. Upande ule kulikokuwa hai kunakufa, na kule kulikokuwa kumekufa kunakuwa hai. Yaani, tunakuwa wafu kwa dhambi, kisha tunakuwa hai kwa Kristo. Kabla ya hapo tulikuwa hai(active) kwenye dhambi, na tulikuwa wafu kwa haki/Kristo, hata kama tulikuwa watenda mema. *Swali ni je! TUNAKUFAJE SASA?* Sio tu tunakufaje, bali pia Biblia imeeleza tunazikwaje. Wakati mtu anapomwamini Yesu kama Mwokozi na kutubu, hapo ndipo utu wa kale au kwa maneno rahisi mwili wa dhambi unasulibiwa pamoja na Yesu na kuuawa pale msalabani.

 Yaani, kile kile Yesu alichofanyiwa hadi akafa msalabani, ndicho hicho kinachotendwa kwa mwili wa dhambi. Sasa, Yesu hakubaki msalabani, bali alizikwa. Hivyo, hata huu mwili wa dhambi/utu wa kale nao unatakiwa kuzikwa. *MWILI WA DHAMBI UNAZIKWAJE?* Ni katika tendo la ubatizo, ndio maziko hufanyika. Ndio maana ni ajabu sana ukitaa kubatizwa kwa kuzikwa kwenye maji baada ya kutubu. Ndio hapa Biblia hutaja neno ubatizo kama maziko(mlizikwa na Kristo kwa njia ya ubatizo). Lakini kumbuka, Yesu hakukaa kaburini daima. Alifufuka. Ndio maana tunapobatizwa hatuachwi huko kwenye maji. Tunatolewa, ishara ya kuwa TUNAFUFULIWA PAMOJA NA KRISTO. Hapa ndipo Biblia hutuambia, kwa vile Yesu aliacha yale madhambi yetu kaburini, akafufuka na utu mpya, na sisi ndio hivyo hivyo tunapozamishwa/tunapozikwa kwenye maji tunazika utu wa kale, na tunapotolewa, tunakuwa tumefufuka na utu mpya, ama upya wa uzima, kama Biblia inavyosema. Maneno yote niliyoongea hapa, yamefungwa kwenye haya Maandiko: Warumi 6:3-5,8. *Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?* *Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.* *Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;*

 *Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye;* Kwa hiyo, tuseme tu kwa ufupi, KUIFIA DHAMBI NI KUMWAMINI YESU, KISHA KUTUBU KWA KUMAANISHA KUACHA DHAMBI, KISHA KUSHIRIKI TENDO LA UBATIZO WA KIBIBLIA.

 Kuanzia hapa, utakuwa umeokoka, utaombewa ujazo wa Roho Mtakatifu. Anza kuukulia wokovu katika kanisa mojawapo la waliookoka utakalochagua kujiunga nalo.
Axact

Tanzania Worships

Haleluyah! Karibu katika ukurasa wa Tanzania Worships ambao ni maalumu kwa ajili ya kusambaza na kulihubiri Neno la Mungu anayeishi. je kuna maoni na ushauri unataka kuuutoa ili kuhakikisha ukurasa huu unawafikia waamini na wasioamini? basi usione shaka kuwasiliana nasi kwa njia ya mitandao ya kijamii

Post A Comment:

0 comments: