Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Rafiki yangu mmoja siku moja aliniuliza swali lifuatalo ambapo majibu yangu ndio somo la leo, rafiki yangu huyo aliniandikia hivi "Bwana Yesu asifiwe. Samahani mtumishi naomba kuuliza kwamba kuna faida kufanya mapenzi kabla ya ndoa?  Mimi ni binti na kiukweli kuna mtu nilikubaliana nae kuwa tutafunga nae ndoa sasa ananiomba kufanya nae mapenzi kabla ya ndoa na mi sitaki kufanya kwa sasa mpaka nifunge ndoa, ananisumbua sana na sitaki kumpoteza je  nifanyaje Mtumishi?"

Majibu yangu kwa binti huyo yalikuwa ni haya hapa chini, na naomba majibu haya yakusaidie na wewe ambaye hujaingia katika ndoa, kama uko katika ndoa tayari basi somo hili likupe msukumo wa kuwasaidia ambao hawajaingia katika ndoa ili wasikosee na kama na wewe ulikosea basi tubu maana madhara ya dhambi za uchumba yanaweza kukufuatilia hadi ukiwa ndani ya ndoa.

Majibu yangu yalikuwa ni haya:

Hakuna faida hata moja kufanya mapenzi kabla ya ndoa.

Kufanya mapenzi kwa watu ambao hawajafunga ndoa unaitwa "Uasherati" na Biblia iko wazi sana kwamba kwa wateule wa KRISTO wanaojitambua basi uasherati hautakiwi kuwapo kwao.

Waefeso 5:3 "Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"

 Usikubali kamwe kukutana naye Kimwili kabla ya ndoa, ukikubali kufanya naye mapenzi ujue hatakuoa,atakuchukia bila sababu maana shetani atapanda magugu ambayo yatakushinda kuyang'oa, hata ikitokea mmeoana ujue huyo mwanaume hatakuheshimu.

Mfano ni huu.

2 Samweli 13:1-2 " Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote."


Kijana Amnoni alimpenda sana Binti aitwaye Tamari  na upendo ule ulimsumbua sana sana maana alimpenda mno.

Lakini baada ya kufanya naye uasherati ilikuwa hivi

2 Samweli 13:14-15 " Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako."

Baada ya Amnoni kumdanganya Tamari na kufanya naye uasherati akamchukia na kumfukuza, Biblia inasema akamchukia kwa machukio makuu kuliko upendo aliompenda kwanza.

Mahusiano nje ya ndoa

Inawezekana na wewe baada ya kukubali kuzini naye atakuchukia na hatakuoa, lakini pia hata ikitokea mkaoana hakutakuwa na amani katika ndoa maana roho ya chuki kiroho huwa bado ipo, na zipo ndoa nyingi zinateseka na hili, na kumbe chanzo ni uasherati kipindi cha kabla ya ndoa.

Ni jambo baya sana kwa wachumba kukutana kimwili kabla ya ndoa, pia kuruhusu ngono wakati hamko kwenye ndoa kunazalisha roho ya usaliti. 

Ukiruhusu kukutana naye kimwili ujue kitakachofuata ni yeye kukukinai wewe hivyo mlikuwa mfunge ndoa mwakani utashangaa mko wachumba miaka 5, kila ukimwambia mfunge ndoa anakuambia msubiri kwanza maana anakuchunguza kwanza, sasa mtachunguzana hata zaidi ya miaka 5 bila kufunga ndoa wakati alipokujia mwanzo alisema "Amefunuliwa hivyo ana uhakika 100% wewe ni wake na hana mashaka na wewe" sasa mashaka yalianza lini hata atake muanze kuchunguzana? Ni baada ya uasherati.

Mithali 6:32-33 "Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika."

Ukiruhusu  uasherati ujue baada ya hapo hatakwamimi, atakuona wewe rahisi sana hivyo kama umekubali kutembea naye basi shetani atamfanya ajue kwamba wewe ni mrahisi sana na unaweza kumkubalia yeyote kama ulivyomkubalia yeye, kumbuka shetani ni baba wa uongo 

hivyo atajaza uongo kichwani mwa mchumba wako au kichwani kwako pia ili kuua mahusiano hayo.

 Usiruhusu kuwa karibu na mchumba wako mkiwa wawili tu, mshauri afanye taratibu za kufunga ndoa na sio taratibu za ngono.

 Unajua mapando ambayo shetani anaweza kuyapanda kama ukifanya uasherati na mchumba wako? 

1. Mchumba wako atakuchoka.

2. Mchumba wako  atakuona wewe ni  wa kawaida sana maana huna jipya tena kwake.  

3. Mchumba wako atakuona huna akili, atakuona wewe mrahisi sana hivyo unaweza kuwakubaria na wengine.

4. Mchumba wako  atajiona amekuweza hata mkiachana hatakuwa na hasara, akili yake itahamia kwa mwanamke mwingine maana wewe ameshakuona na kukujua.

5. Mchumba wako kiu ya kuoa wewe  itaondoka ndani yake. 

Ndugu,  moja ya vitu hatari sana vya  kuviepuka ni uasherati na uzinzi. 

Nakuomba usikubali kamwe kufanya ngono na mtu ambaye hamjafunga naye ndoa. 

Usikubali kamwe kufanya ngono na mchumba wako. 

Usikubali kamwe kuwa mzinzi na mwasherati.  

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

0 7 1 4 2 5 2 2 9 2(Hadi whatsapp).

0 7 8 6 7 1 9 0 9 0

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe ujumbe huu kama ulivyo.

Axact

Tanzania Worships

Haleluyah! Karibu katika ukurasa wa Tanzania Worships ambao ni maalumu kwa ajili ya kusambaza na kulihubiri Neno la Mungu anayeishi. je kuna maoni na ushauri unataka kuuutoa ili kuhakikisha ukurasa huu unawafikia waamini na wasioamini? basi usione shaka kuwasiliana nasi kwa njia ya mitandao ya kijamii

Post A Comment:

0 comments: